Wabunge kadhaa wa Marekani wameanza kutoa wito wa kumwondoa madarakani Rais Donald Trump kwa kutumia Marekebisho ya 25 ya Katiba ya Marekani, ambayo yanaruhusu kuhamishwa kwa madaraka ikiwa rais atashindwa kutekeleza majukumu yake.
Mbunge wa Arizona kupitia chama cha Democratic, Yassamin Ansari, ni miongoni mwa waliojitokeza karibuni zaidi kuunga mkono hatua hiyo.
Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X, alisema Trump anaongeza kasi ya vita “haramu na yenye madhara makubwa,” akitishia kufanya uhalifu mkubwa wa kivita na kulenga miundombinu ya kiraia nchini Iran. Aliongeza kuwa katika saa 48 zilizopita, matamshi ya rais huyo “yamevuka mipaka yote.”
Awali, Mbunge Ilhan Omar wa Minnesota (Democratic) pia alikosoa vitisho vya Trump dhidi ya miundombinu ya kiraia ya Iran, akisema, “Kiongozi huyu asiye na utulivu lazima aondolewe madarakani.”
Mbunge Melanie Stansbury wa New Mexico (Democratic) naye alitoa wito huo, akisema, “Ni wakati wa Marekebisho ya 25. Bunge na Baraza la Mawaziri lazima wachukue hatua.”
Aliyekuwa mbunge wa chama cha Republican kutoka Illinois, Joe Walsh, pia alitoa kauli kali akisema Trump “atabaki doa kwa nchi hii na dunia,” na kusisitiza Marekebisho ya 25 yatumike mara moja.
Seneta wa chama cha Democratic, Chris Murphy, naye aliandika kuwa kama angekuwa katika Baraza la Mawaziri la Trump, angetumia muda wa Pasaka kushauriana na wanasheria wa katiba kuhusu Marekebisho ya 25. Alisema, “Hali hii haina mantiki kabisa. Tayari amesababisha vifo vya maelfu, na ataendelea kusababisha zaidi.”