Mfanyabiashara bilionea Gautam Adani ameshtakiwa na Marekani kwa madai ya hongo na mpango wa udanganyifu unaofikia dola milioni 265- Tsh Bilioni 703+.
Waendesha mashtaka wa Marekani walidai kuwa Adani, mpwa wake Sagar Adani, na washtakiwa wengine sita walilipa hongo kwa maafisa wa serikali ya India ili kupata kandarasi za usambazaji wa nishati ya jua na kutoa faida ya dola bilioni 2 kwa miaka 20.
Adani na wengine wamefunguliwa mashtaka na Tume ya Usalama na Ubadilishanaji Fedha ya Marekani (SEC) mjini New York kwa madai ya kukiuka Sheria ya Ufisadi wa Kigeni (FCPA). Malalamiko yaliwasilishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Marekani kwa Wilaya ya Mashariki ya New York.
"Wakati wa madai ya mpango huo, Adani Green alikusanya zaidi ya dola milioni 175 kutoka kwa wawekezaji wa Amerika, na hisa za Azure Power ziliuzwa kwenye Soko la Hisa la New York," taarifa rasmi kwa vyombo vya habari ilisema.