Msanii #AngéliqueKidjo atakuwa msanii wa kwanza kutoka Afrika kupewa nyota kwenye Hollywood Walk of Fame.
Tangazo hili lilitolewa rasmi tarehe 2 Julai 2025 na Hollywood Chamber of Commerce, ambapo #Kidjo ametajwa kuwa miongoni mwa watu 35 watakaotuzwa nyota hiyo mwaka 2026. Anaungana na mastaa wengine wa kimataifa kama Miley Cyrus, Rami Malek, Deepika Padukone, na Lea Salonga.
#AngéliqueKidjo ni mwanamuziki mashuhuri wa Benin anayejulikana kwa kuchanganya Afrobeat, jazz, muziki wa jadi wa Kiafrika na mitindo ya kisasa ya kimataifa. Pia ni mshindi wa tuzo nyingi za Grammy na ni mtetezi mkubwa wa haki za binadamu na wanawake duniani.
Kutoa heshima hii ni tukio la kihistoria, kwani licha ya mchango mkubwa wa wasanii kutoka Afrika kwa miongo mingi, hakuna hata mmoja aliyewahi kupata nyota katika barabara hii maarufu hadi sasa.
Tukio rasmi la kutunukiwa nyota bado halijapangwa, lakini kwa mujibu wa taratibu, waheshimiwa waliotajwa wana muda wa miaka miwili kupanga sherehe yao rasmi baada ya kupitishwa na bodi tarehe 25 Juni 2025.