Waziri Mkuu Asimamishwa Kisa Sauti zake Kuvuja

-rickmedia: Lanka Ting

Lanka Ting

7 hours ago
rickmedia: waziri-mkuu-asimamishwa-kisa-sauti-zake-kuvuja-812-rickmedia

Mahakama ya Katiba ya Thailand imemsimamisha kazi Waziri Mkuu, akikabiliwa na shinikizo kubwa la kujiuzulu baada ya tukio la kuvujishwa kwa mazungumzo yake ya simu na kiongozi wa zamani wa Cambodia, Hun Sen.

Mazungumzo hayo yaliyovujishwa, yamezua hasira miongoni mwa raia wa Thailand wengi wao wakiwasilisha ombi la kutaka afutwe kazi jambo ambalo Mahakama imelizingatia.

Waziri Mkuu huyo Paetongtarn Shinawatra ni mwanasiasa wa tatu katika ukoo wenye nguvu wa Shinawatra - ambao umetawala siasa za Thailand kwa miongo miwili iliyopita na kupoteza mamlaka kabla ya kumaliza muda wao.

Muungano wake unaotawala tayari una idadi ndogo ya wabunge baada ya mshirika mkuu wa kihafidhina kujiondoa wiki mbili zilizopita.

Mahakama ya Kikatiba ilipiga kura 7-2 kumsimamisha kazi wakati wakizingatia kesi ya kufutwa kwake na ana siku 15 za kuwasilisha utetezi wake.

Huku hayo yakijiri naibu Waziri Mkuu Suriya Jungrungruangkit atahudumu kama kaimu kiongozi wa nchi.

Ikiwa atafukuzwa kazi, Paetongtarn atakuwa waziri mkuu wa pili kutoka chama cha Pheu Thai kuondolewa madarakani tangu Agosti mwaka jana.