Mtoto wa kiingereza aliyefungwa jela huko Dubai kwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtalii mwenzake kutoka Uingereza aliyekutana naye wakati wa likizo, ameachiliwa kutoka gerezani baada ya miezi saba.
Kundi la kampeni la Detained in Dubai limethibitisha kuwa Marcus Fakana, mwenye umri wa miaka 19, amepokea msamaha wa kifalme kutoka kwa mtawala wa Dubai, Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum.
Marcus, kutoka Tottenham, kaskazini mwa London, alirejea Uingereza siku ya Alhamisi, Julai 3, baada ya kutumikia kifungo chake katika Umoja wa Falme za Kiarabu.
Marcus alikamatwa na kufungwa mwaka 2024, kutokana na uhusiano wa kimapenzi wa hiari na mtalii mwingine wa Kiingereza ambaye alikuwa na umri wa chini kidogo kuliko yeye. Msichana huyo alikuwa mwezi mmoja tu kabla ya kutimiza miaka 18, lakini kufanya mapenzi na mtu yeyote aliye chini ya miaka 18 ni kosa katika nchi hiyo ya Ghuba.
Walikutana wakati familia zao zote mbili zilikuwa zikikaa katika hoteli ya kifahari. Mama wa msichana huyo aliripoti tukio hilo kwa mamlaka za UAE baada ya kuona ujumbe kati yao alipokuwa amerejea Uingereza.
Kesi ya Marcus ilizua hisia na hasira kubwa, ikionyesha sheria kali za UAE zinazokataza mahusiano ya kibinafsi ambazo wakosoaji wanasema huwaathiri zaidi raia wa kigeni.
.
Radha Stirling, Mkurugenzi Mtendaji wa Detained in Dubai, aliambia MailOnline kuwa kuachiliwa kwa Marcus kutoka Gereza la Al Awir kulikuja wiki chache baada ya maombi ya msamaha wa kifalme kuwasilishwa.