Sean "Diddy" Combs anakabiliwa na madai mapya ya unyanyasaji wa kijinsia yaliyoibuliwa katika kesi iliyowasilishwa Jumanne usiku. Madai hayo yanahusiana na matukio tofauti yaliyotokea kati ya 2004 mpaka 2022.
Kwenye tukio moja, mlalamikaji mwenye umri wa miaka 39 alidai kushambuliwa nyumbani kwa Diddy jijini New York mwaka 2022 baada ya kuleweshwa kwa kinywaji kilichokuwa na kitu cha kumfanya apoteze fahamu. Alidai alipoamka, alimkuta Diddy akimfanyia vitendo vya kingono bila ridhaa yake.
Mlalamikaji mwingine alidai kushambuliwa mwishoni mwa miaka ya 1990 baada ya kualikwa New York kwa ajili ya kupewa nafasi kwenye video ya muziki. Mwanamke wa tatu, aliyekuwa na miaka 17 mwaka 2004, alisema alinyanyaswa kijinsia na Diddy kwenye sherehe ya Siku ya Uhuru huko Hamptons.
Mawakili wa Diddy wamepinga madai hayo, wakisema ni njama za kupotosha na kulazimisha malipo kutoka kwa watu maarufu. Walisisitiza kwamba Diddy ana imani na mfumo wa sheria na ukweli utadhihirika kuwa hakuwahi kuwanyanyasa kijinsia watu wowote, wawe wanaume au wanawake, wakubwa au watoto.