Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limethibitisha kutokea kwa tukio la kuawa kwa aliyekuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kilolo Christina Kibiki kwa kupigwa risasi.
Kamanda Bukumbi ametoa taarifa hiyo leo Novemba 13, 2024 ambapo amesema Marehemu alishambuliwa kwa kupigwa risasi kifuani pamoja na kupigwa na kitu kizito kichwani na Watu Wasiofahamika.
"Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa marehemu alivamiwa na vijana watatu wasiofahamika katika nyumba anayoishi na binti zake wawili.
Ameongeza kuwa "watu hao walimshambulia binti mmoja wa marehemu na kumuumiza usoni pamoja na jirani yake ambaye naye ameumizwa eneo la ubavu wa kushoto kwa kupigwa na kitu butu alipokwenda kutoa msaada baada ya kusikia kelele kutoka kwa binti wa marehemu" amesema Kamanda Bukumbi
Kamanda Bukumbi amesema baada ya kufanya shambulio hilo, watu hao walitoroka na hawakuchukua chochote.
"Tunaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na juhudi zinaendelea kuhakikisha watuhumiwa wanapatikana ili wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria"Alisema
Tukio hilo la limetokea usiku wa Novemba 12, 2024 saa tatu Usiku nyumbani kwa Marehemu Mtaa wa Banawano kata ya Mseke, Tosamaganga.