Chris Brown kuendelea kusota Rumande Manchester

-rickmedia: Saraphina Jerry

Saraphina Jerry

22 hours ago
rickmedia: chris-brown-kuendelea-kusota-rumande-manchester-583-rickmedia

Chris Brown, ataendelea kusota hadi tarehe 13 Juni, akikabiliwa na shtaka la kushambulia kwa nia ya kusababisha madhara makubwa ya mwili.

Brown, mwenye umri wa miaka 36, anadaiwa kumshambulia mtayarishaji wa muziki Abraham Diaw kwa kutumia chupa ndani ya klabu ya Tape katikati ya jiji la London mwezi Februari 2023. Waendesha mashtaka wamedai kuwa shambulio hilo lilikuwa la ghafla na lilitokea ndani ya klabu iliyokuwa na watu wengi.

Katika kikao cha mahakama kilichofanyika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Manchester, mwendesha mashtaka Hannah Nicholls alisema Brown alimshambulia Diaw kwa kumpiga kwa chupa mara kadhaa, kisha kumkimbiza na kuendelea kumpiga kwa ngumi na mateke. Tukio hilo lilinaswa kwenye kamera za ulinzi (CCTV).

Brown alifika mahakamani akiwa amevaa suruali za michezo na fulana nyeusi, akiwa na nywele zake zenye rangi ya blonde. Alithibitisha jina lake na tarehe ya kuzaliwa lakini hakukubali wala kukataa kosa.

Hakimu Joanne Hirst alisema kuwa kosa hilo ni kubwa mno kushughulikiwa na mahakama yake, na kuamuru kesi hiyo ihamishiwe katika Mahakama Kuu ya Southwark jijini London.

Brown anatarajiwa kufika huko kwa ajili ya kikao cha kuandaa utetezi tarehe 13 Juni. Maombi yake ya dhamana yalikataliwa.

Msanii huyo alikamatwa na maafisa wa Metropolitan Police alfajiri ya Alhamisi akiwa kwenye hoteli mjini Manchester. Wawakilishi wake bado hawajatoa tamko rasmi kuhusu tukio hilo.

Mashtaka haya yanakuja wakati Brown alikuwa anajiandaa kuanza ziara yake ya kimataifa, inayotarajiwa kuanza Uholanzi tarehe 8 Juni, ikiwa ni pamoja na onyesho la Manchester lililopangwa kufanyika tarehe 15 Juni katika ukumbi wa Co-op Live Arena.

Kabla ya kikao cha mahakama, Naibu Mwendesha Mashtaka Mkuu wa CPS London North, Adele Kelly, alikumbusha umma kwamba kesi dhidi ya mshtakiwa bado iko hai kisheria.

Alisisitiza umuhimu wa watu kujiepusha na kutoa taarifa au maoni mtandaoni ambayo yanaweza kuathiri haki ya mshtakiwa kupata mchakato wa haki wa kisheria.