Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza kuanzishwa kwa majimbo mapya ya uchaguzi manane katika mikoa mbalimbali, huku Mkoa wa Mbeya, jimbo la Mbeya Mjini likigawanywa na kuanzishwa Jimbo la Uyole.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 12, 2025 jijini Dodoma, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji wa Rufani, Jacobs Mwambegele amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mamlaka ya tume katika kurekebisha mipaka ya majimbo ya uchaguzi nchini.
“Baada ya kupokea maombi, tume ilitembelea na kufanya vikao na wadau katika baadhi ya majimbo yaliyoomba kugawanywa na majimbo yote yaliomba kubadilishwa majina, ili kujiridhisha na taarifa za maombi zilizowasilishwa tume,” amesema.