Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) limetangaza kuwa linafuatilia kwa umakini mkubwa mlipuko wa ghasia za magenge ya dawa za kulevya (cartels) nchini Mexico, nchi inayotarajia kuwa mwenyeji mwenza wa fainali za Kombe la Dunia msimu huu wa joto.
Hali ya usalama nchini humo imetikisika kufuatia operesheni ya jeshi iliyopelekea kuuawa kwa Nemesio Oseguera Cervantes, maarufu kama 'El Mencho', ambaye alikuwa kiongozi wa genge hatari la Jalisco New Generation (CJNG). Kifo chake kimezua mashambulizi ya kulipiza kisasi, ambapo wanachama wa genge hilo wameingia mtaani kupambana na jeshi, kufunga barabara, na kuchoma moto magari.
Athari kwa Michuano ya Kombe la Dunia
Hofu kubwa imetanda kutokana na ukweli kwamba mji wa Guadalajara, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Jalisco, umepangwa kuandaa mechi nne za michuano hiyo mikubwa duniani. Aidha, miji mingine ya Mexico City na Monterrey inatarajiwa kuandaa mechi tano na nne mtawalia.
Msemaji wa FIFA amesema kuwa shirikisho hilo liko katika mawasiliano ya kudumu na mamlaka za Mexico:
"Tutaendelea kufuata hatua na maelekezo kutoka kwa vyombo mbalimbali vya serikali, vinavyolenga kudumisha usalama wa umma na kurejesha hali ya kawaida. Tunasisitiza ushirikiano wetu wa karibu na mamlaka za shirikisho, majimbo, na serikali za mitaa."
Pamoja na matamshi hayo ya FIFA, wadau wa michezo duniani wanaendelea kuhoji ikiwa hali hiyo ya usalama itatengemaa kabla ya kuanza kwa fainali hizo, ikizingatiwa kuwa mashabiki mamilioni wanatarajiwa kumiminika nchini humo.