Serikali imetangaza kupanda kwa gharama za vipimo vya Vinasaba vya Binadamu (DNA) kutoka Sh100,000 hadi Sh212,000 kwa sampuli moja, kutokana na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji wa mchakato wa vipimo hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 11, 2026, jijini Dodoma, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, amebainisha kuwa gharama hiyo mpya bado imebakiza ruzuku kubwa kutoka kwa serikali ili kumpunguzia mzigo mwananchi.
“Gharama halisi kwa sampuli moja ilipaswa kuwa kati ya Sh700,000 hadi Sh800,000, lakini kiasi kinachobaki kinalipwa na Serikali ya Tanzania,” alifafanua Dkt. Mafumiko.
Kwa mujibu wa utaratibu huo, kwa kesi ya kawaida inayohusisha baba, mama, na mtoto, gharama ya jumla itakuwa ni Sh636,000 (sawa na sampuli tatu). Maelezo hayo yametolewa katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo, Mtumba, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa ofisi hiyo kutoa ufafanuzi wa huduma za kimaabara nchini.