Trump anasema Saudi Arabia lazima iitambue Israel

-rickmedia: Saraphina Jerry

Saraphina Jerry

2 hours ago
rickmedia: trump-anasema-saudi-arabia-lazima-iitambue-israel-236-rickmedia

Rais wa Marekani Donald Trump amesema makubaliano ya nyuklia kati ya Marekani na Saudi Arabia yatatekelezwa tu ikiwa Saudi Arabia itaitambua rasmi Israel na kujiunga na Makubaliano ya Abraham (Abraham Accords).

Trump ametoa kauli hiyo kupitia mtandao wake wa Truth Social kuwa makubaliano hayo yanahusu matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia pekee na hayatakuwa na urutubishaji wa nyenzo za nyuklia.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa makubaliano hayo hayataidhinishwa bila Saudi Arabia kujiunga na Makubaliano ya Abraham yanayolenga kuimarisha uhusiano kati ya Israel na baadhi ya mataifa ya Kiarabu.

Msemaji wa Ikulu ya White House, Karoline Leavitt, amesema Trump amekuwa akiwaeleza viongozi wa Saudi Arabia mara kwa mara kuhusu sharti hilo.

Alisema msimamo wa Rais Trump ni kwamba bila Saudi Arabia kujiunga na Makubaliano ya Abraham, makubaliano ya nyuklia hayatatekelezwa.

Kauli hizo zimeibua mjadala baada ya wataalamu na baadhi ya wabunge wa Marekani kuonya kuwa makubaliano hayo yanaweza kuongeza hatari ya kuenea kwa teknolojia ya nyuklia katika Mashariki ya Kati, eneo ambalo tayari linakabiliwa na migogoro ya kiusalama.