Mtangazaji na mtayarishaji wa vipindi vya televisheni nchini Misri, Sarah Khalifa (39), amehukumiwa kifo kwa kunyongwa pamoja na washtakiwa wengine 11 katika kesi kubwa ya dawa za kulevya iliyofikishwa katika Mahakama ya Jinai ya Cairo.
Khalifa anafahamika zaidi kwa kuendesha kipindi cha “Mission Impossible”, kilichojikita katika masuala ya uhalifu na usalama.
Kwa mujibu wa taarifa za mahakama, Khalifa na washtakiwa wenzake walipatikana na hatia ya kuunda mtandao wa uhalifu uliopangwa, uliodaiwa kuhusika na uingizaji wa malighafi zilizotumika kutengeneza dawa za kulevya kwa ajili ya biashara, pamoja na makosa mengine yanayohusiana na umiliki wa silaha na risasi bila leseni.
Mamlaka ziliripoti kuwa, katika uchunguzi huo, zilikamata zaidi ya kilo 750 za dawa za kulevya na malighafi, huku maeneo mawili yakidaiwa kutumika kama maabara za kutengeneza dawa hizo.
Kesi hiyo ilikuwa na washtakiwa 28 kwa jumla. Mbali na watu 12 kuhukumiwa kifo, wengine tisa wamehukumiwa kifungo cha maisha, huku saba wakiachiliwa huru.
Hukumu hiyo ilitolewa baada ya mahakama kupata maoni ya Mufti Mkuu wa Misri, hatua inayohitajika katika kesi zinazoweza kupelekea hukumu ya kifo nchini humo. Hata hivyo, hukumu hiyo inaweza kukatiwa rufaa.
Sarah Khalifa amekuwa akikana kuhusika na tuhuma hizo. Wakati wa kutolewa kwa hukumu hiyo, alisisitiza kuwa hana hatia.