Wanne wafariki kwenye ajali Bunju Jijini Dar Es Saalam

-rickmedia: Saraphina Jerry

Saraphina Jerry

52 minutes ago
rickmedia: wanne-wafariki-kwenye-ajali-bunju-jijini-dar-saalam-601-rickmedia

Watu wanne wamefariki dunia kufuatia ajali ya basi kugongana na gari ndogo aina ya Toyota IST, iliyotokea usiku wa Septemba 7, 2026, saa 07:40, katika barabara ya Bagamoyo, eneo la Bunju Sokoni, Kinondoni, Dar es Salaam.

Ajali hiyo ilihusisha basi mali ya kampuni ya Abood, lililokuwa likiendeshwa na Christivian Steven Shemuhilu (38), mkazi wa Kange, Tanga, likitokea Tegeta kuelekea Bunju kwenda mkoani Tanga. Basi hilo liligongana na gari aina ya Toyota IST, lililokuwa likiendeshwa na Hamad Mohamed Juma maarufu Majid (37), mkazi wa Mtoni Mtongani, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi, Jumanne Muliro, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari kwa watumiaji wengine wa barabara.

Ajali hiyo imesababisha vifo vya Majid, Edward Kimanyara, mkazi wa Yombo Dovya, Dar es Salaam, Magdalena Manyenga (45), mkazi wa Temeke, Dar es Salaam na Melina Emmanuel Kayoka (42), mkazi wa Yombo Kisiwani, Temeke, Dar es Salaam.

Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala, Kinondoni, huku dereva wa basi akishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa hatua nyingine za kisheria.

Jeshi la Polisi limetoa wito kwa watumiaji wa barabara, wakiwemo waendesha vyombo vya moto, kuendelea kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani ili kuzuia na kuepusha ajali zinazoweza kusababisha vifo na madhara kwa watumiaji wa barabara.