Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amekaribisha tangazo la kusitisha mapigano kwa muda wa wiki mbili kati ya Marekani na Iran.
Kupitia msemaji wake, Guterres ametoa wito kwa pande zote kuheshimu sheria za kimataifa na masharti ya makubaliano hayo, akisisitiza kuwa sitisho hilo ni muhimu kulinda maisha ya raia na kupunguza mateso ya kibinadamu yanayosababishwa na vita.
Aidha, Guterres alithamini juhudi za upatanishi zilizofanywa na nchi mbalimbali, ikiwemo Pakistan, katika kufanikisha makubaliano hayo.
Ujumbe huo unakuja huku juhudi za kidiplomasia zikiendelea kufanikisha makubaliano ya kudumu yatakayorejesha utulivu katika eneo la Mashariki ya Kati.