Hatimaye mpenzi wa mhamasishaji wa mitandao ya kijamii kutoka Marekani, Ashly Robinson, maarufu Ashlee Jenae, Joe McCann anahojiwa na polisi visiwani Zanzibar.
Ashlee, alifariki dunia Aprili 10, mwaka huu visiwani Zanzibar alikokwenda kwa matembezi ya kitalii na mpenzi wake, Joe McCann, ambaye alimchumbia siku sita kabla ya kifo chake wakiwa visiwani humo.
Taarifa kuhusu kuhojiwa kwa mpenzi wake huyo, imetolewa leo, Jumanne Aprili 14, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Benedict Mapujira, alipozungumza na Mwananchi.
Katika taarifa yake hiyo, amesema pamoja na uchunguzi ambao tayari ulishafanyika, lazima jeshi hilo liendelee na mahojiano kujiridhisha kama kuna jinai, hivyo inawahoji watu kadhaa.
“Lazima tuhoji watu wa hotelini, tumuhoji yule mchumba wake, kila kitu ili baadaye tupate hitimisho kama kuna jinai au hatuna jinai,” amesema na alipoulizwa kuhusu alipo McCann alijibu, bado anahojiwa.
Alipoulizwa zaidi kama wanamshikilia McCann, Kamanda Mapujira amejibu, “unajua ukiambiwa unaisaidia polisi unakuwa umebanwabanwa, hata kama una uhuru lakini ukiambiwa unaisaidia polisi taabu.”