Waandishi wa habari watatu wa Kipalestina wameuawa katika shambulio la Israel katikati mwa Gaza, kwa mujibu wa wahudumu wa uokoaji.
Shirika la Ulinzi wa Raia la Gaza linaloendeshwa na Hamas lilisema gari lao lilipigwa katika eneo la al-Zahra, na likawataja waliouawa kuwa ni Mohammed Salah Qashta, Anas Ghneim na Abdul Raouf Shaat. Inaelezwa kuwa walikuwa wakifanya kazi kwenye shirika la misaada kutoka Misri.
Jeshi la Israel lilisema lilishambulia washukiwa kadhaa waliokuwa wakiendesha droni inayohusishwa na Hamas kwa namna iliyotishia askari wake na kuongeza kuwa tukio hilo bado linachunguzwa.
Watu wengine wanane, wakiwemo watoto wawili, pia waliuawa na mizinga na risasi za Israel katika maeneo mbalimbali ya Gaza siku ya Jumatano, kulingana na wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas.