Urusi imezua taharuki mpya ya kidiplomasia Jumanne hii kwa kuishutumu Ukraine kwa jaribio la kutaka kumiliki silaha za nyuklia kwa msaada wa Uingereza na Ufaransa, madai ambayo Kyiv imeyataja kuwa "uongo wa kipuuzi."

Katika taarifa iliyotolewa na Idara ya Ujasusi wa Kigeni ya Urusi (SVR) ikiadhimisha miaka minne tangu kuanza kwa vita hivyo, Moscow imedai kuwa Uingereza na Ufaransa zinaamini kuwa Ukraine itapata nguvu zaidi ya majadiliano ya kumaliza vita ikiwa itamiliki "bomu la nyuklia" au angalau lile linalojulikana kama "dirty bomb."
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Ufaransa ameyataja madai hayo kama "upotoshaji wa wazi." huku msemaji wa Mambo ya Nje wa Ukraine Heorhii Tykhyi, amesisitiza kuwa Ukraine imekuwa ikikanusha madai hayo ya kipuuzi mara kwa mara na inaendelea kufanya hivyo".
SVR imedai kuwa Uingereza na Ufaransa "zinafanya kazi kwa bidii" kutoa silaha hizo huku zikijaribu kuficha mhusika ili ionekane Ukraine imezipata yenyewe, madai ambayo yanaonekana kuzidisha hofu ya kuongezeka kwa makali ya vita hivyo yanapoingia mwaka wa tano.