Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha hadi Juni 2, 2025 kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu baada ya upande wa Mashtaka kusema kuwa uchunguzi wa shauri hilo bado haujakamilika na kuiomba Mahakama kupanga tarehe nyingine.
Upande wa Serikali katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti huyo wa CHADEMA, umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa zipo hatua za mwisho kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo.
Hata hivyo, Mahakama pia imetoa uamuzi mdogo kwamba kesi hiyo itaendelea kusikilizwa kwa njia ya kawaida na si kwa njia mtandao, huku wanaoudhuria kesi wakitakiwa kuacha mihemko ya kelele mahakamani.
Kesi hiyo ya uhaini ipo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franko Kiswaga ambapo awali Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga aliieleza Mahakama kwamba kesi hiyo imeitishwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika.