Sean "Diddy" Combs anadaiwa kutoroka kwa siri Los Angeles baada ya mauaji ya rapa Notorious B.I.G. Machi 9, 1997, kwa msaada wa maafisa wa LAPD, kulingana na madai mapya ya Kirk Burrowes, mwanzilishi mwenza wa Bad Boy Entertainment.
Kwenye kesi aliyofungua, Burrowes anadai kuwa Diddy, akiwa amepaniki lakini salama, aliharakisha kuondoka badala ya kuwafariji familia ya Wallace au wafanyakazi wa Bad Boy. Burrowes anasema Diddy alimtafuta mfanyabiashara mashuhuri Clarence Avant, ambaye kwa ushawishi wake aliwezesha kutoroshwa kwa Diddy kupitia gari la polisi hadi uwanja wa ndege binafsi.
Kesi hiyo pia inamshutumu Diddy kwa maombolezo ya kinafiki baada ya kifo cha Wallace, ikidai kuwa kwa siri, yeye na wakili wake walimshinikiza Burrowes awape mkataba wa mwisho wa Notorious B.I.G., ambao ulikuwa unampa udhibiti zaidi wa kifedha.
Diddy bado hajajibu rasmi madai haya mazito, lakini kesi hiyo imeongeza shinikizo kubwa dhidi yake katika kipindi hiki ambacho anakabiliwa na tuhuma mbalimbali za unyanyasaji na vitisho.