Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kupitia Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imetangaza kuahirisha Mchezo wa Yanga dhidi ya Simba kwa mujibu wa Kanuni ya 34:1(1.3) ya Ligi Kuu, ili kutoa nafasi ya kupata taarifa zaidi kuhusu malalamiko ya Simba kuhusu kuzuiwa kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Mkapa, jana Machi 7, 2025.
Taarifa ya Bodi imesema inasubiri uchunguzi zaidi ili usaidie kufanya maamuzi ya Haki na kuwa itatoa taarifa kamili kuhusiana na tukio hilo na kutangaza tarehe ya Mchezo huo mapema iwezekanavyo.
Awali, usiku wa kuamkia leo Klabu ya Simba ilitangaza kuwa haitapeleka Timu uwanjani kutokana na tukio hilo ikiwatuhumu baadhi ya Watu wa Yanga kushiriki kuwazuia kuingia Uwanjani. Upande wa pili Yanga ikatoa taarifa kuwa itapeleka Timu uwanjani kama kawaida.