Mtangazaji mashuhuri wa televisheni nchini Mexico, Debora Estrella, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 43 kufuatia ajali ya ndege iliyotokea tarehe 20 Septemba katika eneo la Garcia, Nuevo León.
Debora alikuwa akijifunza kurusha ndege, na alikua na mwalimu wake wa urubani, Bryan Ballesteros, ambaye pia alipoteza maisha katika ajali hiyo. Ndege yao ndogo aina ya Cessna ilianguka karibu na eneo la viwanda muda mfupi baada ya kupaa.
Kampuni ya televisheni ya Multimedia, aliyokuwa akifanya kazi nayo, imethibitisha kifo chake na kueleza masikitiko yao kwa kumpoteza mwandishi huyo aliyekuwa maarufu kupitia kipindi cha Telediario Monterrey na Milenio Televisión.
"Tunatoa pole kwa familia na wapendwa wake. Pumzika kwa amani, rafiki yetu," ilisomeka sehemu ya taarifa ya Multimedia.
Debora alikuwa ameshiriki picha ya ndege aliyokuwa anajifunzia siku hiyo, akiandika: “Guess what”, kabla ya somo lake la mwisho.