Baraza la Mawaziri la Zimbabwe limeidhinisha rasimu ya sheria inayopendekeza mabadiliko makubwa ya Katiba, hatua inayoweza kumruhusu Rais Emmerson Mnangagwa (83) kuendelea kusalia madarakani hadi mwaka 2030 au zaidi.
Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, mfumo wa kumchagua Rais utabadilishwa kutoka kura ya moja kwa moja ya wananchi na badala yake Rais atachaguliwa na Wabunge. Pia, muda wa muhula mmoja utaongezwa kutoka miaka mitano ya sasa hadi miaka saba, huku ukomo ukiwa mihula miwili.
Iwapo mabadiliko hayo yatapitishwa, yanaweza kubadili mwelekeo wa kisiasa wa taifa hilo na kufungua mjadala mpana kuhusu mustakabali wa demokrasia nchini humo.
Akizungumza jana Jumanne, Februari 10, 2026, Waziri wa Sheria wa Zimbabwe, Ziyambi Ziyambi, amesema Serikali itafanya mashauriano ya umma kabla ya kuwasilisha rasmi muswada huo bungeni. Hata hivyo, wataalamu wa sheria wameibua tahadhari wakisema marekebisho yanayogusa ukomo wa muda wa uongozi yanahitaji kura ya maoni ya wananchi wote na si uamuzi wa Bunge pekee.
Wataalamu hao wanasema kisheria na kwa misingi ya demokrasia, mabadiliko ya Katiba yanayohusu ukomo wa mihula hayapaswi kumnufaisha kiongozi aliyepo madarakani wakati marekebisho hayo yanapitishwa.
Mnangagwa aliingia madarakani mwaka 2017 kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyomng’oa aliyekuwa Rais wa muda mrefu, Robert Mugabe. Baadaye alishinda uchaguzi wa mwaka 2018 na 2023.
Kwa mujibu wa Katiba ya sasa iliyopitishwa mwaka 2013, Rais anatakiwa kuhudumu mihula miwili ya miaka mitano mitano, hivyo muhula wa mwisho wa Mnangagwa ulipaswa kumalizika mwaka 2028.