Mama mzazi wa rapa na mfanyabiashara Sean “Diddy” Combs, Janice Combs, ametoa taarifa mpya akikosoa vikali madai yaliyojitokeza kwenye makala ya Netflix Sean Combs: The Reckoning iliyotolewa Disemba 2, 2025.
Kwenye tamko lake, Janice amesema kuwa taarifa zinazohusu malezi na maisha ya familia ya mwanawe zina upotoshaji wa makusudi kwa lengo la kuwapotosha watazamaji na kuharibu heshima ya familia yao.
Janice amekanusha vikali madai kuwa alikuwa mzazi mkatili, akisisitiza kuwa alimlea Diddy kwa upendo, bidii na kujitolea, licha ya changamoto za maisha. Amesema alikuwa mama wa pekee aliyelazimika kufanya kazi zaidi ya moja ili kuhakikisha mwanawe anapata maisha na elimu bora.
Aidha, amekanusha taarifa zilizodai kuwa Diddy aliwahi kumpiga kofi, akieleza kuwa madai hayo ni ya uongo kabisa. Janice amesema kumbukumbu zake kuhusu Diddy ni za mtoto mwenye nidhamu, bidii na malengo makubwa tangu utotoni.
Pia, amewataja watu binafsi waliotoa madai hayo akisema wanatumia matukio ya huzuni ya kihistoria kwa maslahi binafsi na ya kutafuta umaarufu, jambo alilolitaja kuwa ni la kusikitisha na lisilokubalika.
Kauli ya Janice Combs imeibua mjadala mpana mitandaoni, huku wengi wakitafakari kuhusu mipaka ya documentaries na wajibu wake katika kusimulia hadithi nyeti za maisha ya watu mashuhuri.