Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amekosoa matamshi ya hivi majuzi kutoka kwa Marekani kuhusu mzozo wa Ukraine, akidai kuwa Marekani inajaribu "kumfurahisha" Moscow katika juhudi zake za kutafuta suluhisho la vita hivyo.
Katika mahojiano yaliyotangazwa Jumatatu, Februari 17, Zelensky alijibu kauli zilizotolewa na maafisa wa Marekani, akipendekeza kuwa wanajipendekeza sana kwa Rais wa Urusi, Vladimir Putin.
"Marekani sasa inasema mambo yanayomfaidisha sana Putin kwa sababu wanataka kumfurahisha," Zelensky alisema, akirejelea juhudi za Marekani kupata suluhisho la haraka kwa mzozo huo.
Zelensky alikataa wazo la kusitisha mapigano kama ushindi, akisisitiza kuwa Ukraine haitakubali makubaliano yoyote kwa ajili ya kumaliza vita tu.
Katika mahojiano hayo, ambayo yalirekodiwa wakati wa Mkutano wa Usalama wa Munich, Zelensky pia alieleza wasiwasi wake kuhusu uwezo wa kijeshi wa Ulaya, akionya kuwa bara hilo litakuwa hatarini bila msaada wa kiusalama kutoka Marekani. Aliitaja Ulaya kuwa “dhaifu” katika suala la nguvu za wanajeshi, utayari wa kivita, na miundombinu ya kijeshi, akisema kuwa nafasi ya Ulaya haijaimarika sana katika miaka ya hivi karibuni.
Zelensky pia alisisitiza jukumu muhimu la msaada wa Marekani katika uimara wa Ukraine dhidi ya uchokozi wa Urusi. Ingawa Ukraine imekuwa na nguvu zaidi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Zelensky alisisitiza kuwa ushindi wa Ukraine usingewezekana bila msaada endelevu wa Marekani. Aidha, alizungumzia uwezekano wa kupelekwa kwa wanajeshi wa kigeni kusimamia usitishaji wa mapigano siku zijazo, akipendekeza kuwa ushiriki wa Marekani ungekuwa muhimu kudumisha mshikamano kati ya washirika wa Ukraine.
Alipoulizwa ikiwa angejiuzulu kwa ajili ya amani, Zelensky alisema yuko tayari kufanya lolote kuhakikisha mustakabali wa Ukraine, ikiwa ni pamoja na kujiuzulu iwapo nchi hiyo ingepata uanachama wa EU na NATO pamoja na dhamana za usalama. “Ikiwa kesho Ukraine itakubaliwa katika EU na NATO, ikiwa wanajeshi wa Urusi wataondoka na tukapata dhamana za usalama, sitahitajika tena,” aliongeza.