Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga limemkamata askari wa Jeshi la Magereza (Jina limehifadhiwa kwa tuhuma za kumuua mke wake, Betia Chacha, mkazi wa Ibadakuli, kwa kumkata sehemu mbalimbali za mwili kwa kipande cha chupa. Tukio hilo lilitokea Novemba 30, 2025.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, amethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa marehemu alikatwa kwenye mkono, shingo na mapaja na kufariki dunia papo hapo. Chanzo kinadaiwa kuwa wivu wa kimapenzi na migogoro ya kifamilia.
Kamanda Magomi ametoa wito kwa wananchi kuepuka kujichukulia sheria mkononi, huku akisisitiza msimamo wa Jeshi la Polisi kupinga ukatili wa kijinsia katika kipindi cha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa kwa uchunguzi zaidi na mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa kwa hatua za kisheria.