Mganga Ahukumiwa Miaka 30 Jela Kuishi Kama Mke na Mume na Binti wa Miaka 14

-rickmedia: Lanka Ting

Lanka Ting

1 week ago
rickmedia: mganga-ahukumiwa-miaka-jela-kuishi-kama-mke-mume-binti-miaka-998-rickmedia

Fadhili Shaaban ambaye ni mganga wa kienyeji mkazi wa Kijiji cha Bunazi wilayani Missenyi Mkoa wa Kagera amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na kulipa fidia ya shilingi Milioni tatu baada ya kukutwa na kosa la kuishi kinyumba na mtoto wa miaka 14 kama mke wake.

Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Missenyi, Yohana Myomba amesema mahakama imetoa hukumu hiyo baada ya kuridhika na ushahidi usio na shaka uliotolewa na mashahidi watano pamoja na kielelezo kilichotolewa na upande wa mashtaka.

Amesema kutokana na hatua hiyo mshtakiwa alikiuka sheria ya kanuni ya adhabu ya kifungu namba 130 kifungu kidogo cha kwanza na cha pili ambapo imeelezwa mahakamani hapo kuwa mtoto huyo alifikishwa kwa Fadhili ili amtibu kidonda katika mguu wake na baada ya kufanikiwa kumtibu ndipo alipoanza kumfanyia vitendo vya kumuingilia kimwili mara kwa mara huku akimtishia kumdhuru pindi akitoa taarifa za kufanyiwa vitendo hivyo.

Kabla ya kutoa adhabu hiyo mwendesha mashtaka Amon Rutalibatwa aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine huku akiiomba mahakama kuamuru mshtakiwa amlipe fidia muathirika wa tukio hilo.

Alipoulizwa kama ana sababu za kujitetea kabla ya kusomewa hukumu hiyo, mshtakiwa Fadhili Shaaban aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwa sababu ana watoto wadogo wanaomtegemea ambao walitelekezwa na mama yao na kwamba bibi yao anayewalea ni mgonjwa kwa sasa.

Mara baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo ya kifungo cha miaka 30 kwa mshtakiwa, Hakimu Myomba amesema mshtakiwa ana haki ya kukata rufaa ndani ya siku 3O toka hukumu hiyo kutolewa.