Mkazi wa Mtaa wa Karikacha, Kata ya Rau, mkoani Kilimanjaro, Michael Lambau (18) anadaiwa kujiua kwa kujinyonga akiwa mahabusu ya Kituo cha Polisi Moshi kati alikokuwa akishikiliwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo jana Januari 13, 2026.
Aidha, Kamanda Maigwa amesema awali mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari 13, 2026 kwa kosa la kumshambulia na kumpiga kwa bapa la panga baba mdogo wake aitwaye Brian Felix.
"Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linafanya uchunguzi wa tukio la kujiua kwa mtu mmoja aitwaye Michael Lambau (18), mkazi wa Mtaa wa Karikacha, Kata ya Rau Manispaa ya Moshi akiwa mahabusu katika kituo cha Polisi Moshi Kati alikokuwa akishikiliwa kwa kosa la shambulio la kudhuru mwili,"amesema Kamanda Maigwa
Amefafanua, mtuhumiwa alikamatwa Januari 13, 2026 kwa tuhuma za kumshambulia kwa kumpiga na mabapa ya panga Brian Felix ambaye ni baba yake mdogo.