Wakati maziko ya kijana Michael Rambau (19) ambaye polisi wanasema alijiua kwa kujinyonga akiwa Kituo Kikuu cha Polisi mjini Moshi yakifanyila leo, Jumamosi, Januari 17, 2026, maswali 10 tata bado hayajapata majibu juu ya mazingira ya kifo hicho.
Kijana huyo ambaye alikuwa fundi bomba na dereva bodaboda mkazi wa mtaa wa Karikacha, kata ya Rau, mkoani Kilimanjaro anadaiwa kujinyonga kwa kutumia mkanda akiwa mahabusu alikokuwa akishikiliwa Januari 13, 2026 kwa tuhuma za kumjeruhi baba yake mdogo kwa kumpiga bapa la panga.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Januari 14, 2016 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa mtuhumiwa huyo pia alikuwa anatuhumiwa kumuua baba yake mzazi Novemba 22, 2025 kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali shingoni na kisha kutoroka hadi alipokamatwa Januari 13, kwa tuhuma za kumshambulia na kumdhuru baba yake mdogo, Brian Felix.
Msemaji wa familia hiyo, Today Rambau alisema kijana huyo (marehemu) alitofautina na baba yake mdogo, alipochukua spana za gari la marehemu baba yake, aliyefariki Novemba 22, mwaka jana.
Familia hiyo pia ilikana kufahamu tuhuma za kujana huyo kumuua baba yake na kuwa alikuwa ametoroka, suala ambalo linaongeza maswali juu ya tukio hilo.