Maafisa 6 Wamesimamishwa Kazi Kisa Trump Kupigwa Risasi

-rickmedia: Lanka Ting

Lanka Ting

1 day ago
rickmedia: maafisa-wamesimamishwa-kazi-kisa-trump-kupigwa-risasi-677-rickmedia

Maafisa sita wa Kikosi Maalum cha Ulinzi wa Rais wa Marekani (Secret Service) wamesimamishwa kazi kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kuhusiana na jaribio la kumuua aliyekuwa mgombea urais wakati huo, #DonaldTrump, lililotokea mwaka jana huko Butler, Pennsylvania.

Hatua hizo za kinidhamu zimeidhinishwa siku nne kabla ya kumbukumbu ya tarehe 13 Julai 2024, siku ya tukio hilo ambapo #Trump alijeruhiwa kwenye sikio. #CoreyComperatore, ambaye alikuwa ni zimamoto aliyekuwa akihudhuria mkutano wa kampeni wa #Trump siku hiyo, aliuawa katika shambulio hilo.

Wapiga risasi wa kujibu mashambulizi waliokuwa sehemu ya kikosi cha usalama cha #Trump waliuua mshambuliaji huyo, ambaye FBI ilimtambua kama #ThomasMatthewCrooks, mwenye umri wa miaka 20.

Baada ya shambulio hilo, uchunguzi huru uliofanywa na Idara ya Usalama wa Ndani (DHS) ulibaini kuwa kulikuwa na mfululizo wa mapungufu ya utekelezaji wa sheria yaliyosababisha mazingira yaliyomwezesha muuaji kumkaribia #Trump. Ripoti hiyo ilisema, “Secret Service haifanyi kazi katika viwango vya juu vinavyohitajika ili kutimiza jukumu lake nyeti.

Mkurugenzi wa Secret Service wakati huo, Kimberly Cheatle, alijiuzulu siku 10 baada ya shambulio hilo.

Adhabu dhidi ya maafisa hao sita zilitolewa katika miezi ya hivi karibuni, na walipewa haki ya kukata rufaa. Kulingana na afisa mmoja aliyearifiwa kuhusu hatua hizo, adhabu hizo zilihusisha kusimamishwa kazi kwa muda wa kati ya siku 10 hadi 42.

Vyeo vya waliosimamishwa kazi vilianzia kwa wasimamizi hadi maafisa wa mstari wa mbele, kwa mujibu wa chanzo kimoja kilicho karibu na maamuzi ya idara hiyo.

Takribani wiki tisa baada ya tukio la Butler, Trump alipata jaribio la pili la kuuawa wakati alipokuwa akicheza gofu katika uwanja wake huko West Palm Beach, Florida.

Kufuatia matukio yote mawili, mgombea huyo wa urais alipewa ulinzi wa kiwango cha rais huku kampeni yake ikilazimika kuandaa mikakati mipya ya kiusalama kwa ajili ya matukio yake.