Serikali Yalifutia Usajili Kanisa la Askofu Josephat Gwajima

-rickmedia: Lanka Ting

Lanka Ting

3 days ago
rickmedia: serikali-yalifutia-usajili-kanisa-askofu-josephat-gwajima-251-rickmedia

Serikali imetangaza kulifutia usajili Kanisa la Ufufuo na Uzima, linalomilikiwa na Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima, ikiwa ni siku moja tangu kiongozi huyo wa kiroho atangaze msimamo wake wa kuendelea kukemea vitendo vya utekaji na watu kupotea.

Sababu ya uamuzi huo wa Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa ni kile kilichoelezwa, kanisa hilo limekiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Jumatatu Juni 2, 2025 na Kihampa, kitendo kilichofanywa na Askofu Gwajima kinaweza kuhatarisha amani na utulivu nchini.

“Kwa mamlaka niliyopewa, ofisi ya msajili wa jumuiya za kiraia inafuta usajili wa Glory of Christ Church Kanisa la Ufufuo na Uzima, kuanzia leo Juni 2, 2025. Hivyo, unatakiwa kusitisha shughuli za kanisa lako mara moja,” amesema Kihampa kwenye barua hiyo ambayo nakala imetumwa kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillius Wambura.

Wiki moja iliyopita Askofu Gwajima alizungumza na waandishi wa habari, akikemea vitendo vya utekaji, jambo lililozua upinzani kutoka miongoni mwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Jana Jumapili, Juni 1, 2025 katika Ibada pamoja na maombi mengine Askofu Gwajima alitangaza maombi ya siku saba kuanzia leo Jumatatu katika makanisa ya Ufufuo na Uzima zaidi ya 2,000 ya kuombea haki na amani.