Marufuku Kuvuta Sigara Maeneo ya Wazi Kuanzia Julai 1.

-rickmedia: Lanka Ting

Lanka Ting

3 days ago
rickmedia: marufuku-kuvuta-sigara-maeneo-wazi-kuanzia-julai-649-rickmedia

Kuanzia Julai 1, Ufaransa itaanza kutekeleza marufuku ya uvutaji wa sigara katika maeneo ya wazi ya umma yanayoweza kufikika na watoto, ikiwa ni pamoja na fukwe, mbuga, bustani za umma, vituo vya basi, viwanja vya michezo, na maeneo yanayozunguka shule.

Hatua hiyo ilitangazwa na Waziri wa Afya na Familia, #CatherineVautrin, aliyesisitiza umuhimu wa kuwalinda watoto dhidi ya athari za tumbaku.

"Uvutaji wa sigara lazima ukome mahali ambapo kuna watoto," Vautrin aliambia gazeti la Ouest-France, na kuongeza kuwa haki ya kuvuta sigara ina kikomo pale ambapo haki ya mtoto ya kuvuta hewa safi inaanza. Wale watakaokiuka sheria hiyo wanaweza kutozwa faini ya hadi €135 (sawa na $154) (Tsh.401,340).

Sheria hizi mpya zinaendeleza hatua za awali za Ufaransa za kupunguza matumizi ya tumbaku katika miaka ya hivi karibuni. Hata hivyo, marufuku hii haitahusisha maeneo ya viti vya wazi vya migahawa (terraces) wala sigara za kielektroniki, ambazo bado zinatumika sana nchini humo.

Uvutaji wa sigara tayari umepigwa marufuku katika maeneo yaliyofungwa kama sehemu za kazi, viwanja vya ndege, vituo vya treni, na sehemu za kuchezea watoto. Zaidi ya manispaa 1,500 tayari zilikuwa zimeweka marufuku zao za maeneo ya wazi.

Ingawa Ufaransa ina viwango vya juu zaidi vya uvutaji wa sigara barani Ulaya takribani 35% ya watu wake—tafiti za hivi karibuni zinaonyesha kuwa 62% ya raia wa Ufaransa wanaunga mkono marufuku ya uvutaji wa sigara katika maeneo ya umma. Marufuku hii inaendana na Mpango wa Kitaifa wa Kupambana na Tumbaku wa 2023–2027, unaolenga kuunda kizazi kisicho na tumbaku kufikia mwaka 2032.

Wakati makundi yanayopinga tumbaku yakiunga mkono hatua hiyo, awali yalikuwa yamekosoa kuchelewa kwa utekelezaji wake. Vautrin alisema kwa sasa hakuna mipango ya kuongeza kodi ya sigara, akitaja hofu kuhusu kuongezeka kwa biashara ya magendo.