Katika tukio la kushtua, ndege aina ya Beech B200 Super King Air imeanguka muda mfupi baada ya kuruka katika Uwanja wa Ndege wa Southend jijini London.Tukio hilo la kutisha limeonekana kwenye video ambayo kwa sasa inasambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii.
Katika video hiyo, inaonekana mlipuko mkubwa wa moto ulitokea mara baada ya ajali hiyo kutokea.
Huduma za dharura zilikimbilia eneo la tukio baada ya moshi mzito kuonekana ukitoka kwenye mabaki ya ndege iliyokuwa ikiteketea kwa moto. Haijafahamika bado ni watu wangapi walikuwa ndani ya ndege hiyo wakati wa ajali.
Kwa mujibu wa ripoti, ndege hiyo ilikuwa na injini mbili na ilikuwa safarini kuelekea Lelystad nchini Uholanzi. Safari hiyo ilikuwa ipangwe kuanza saa 9:45 alasiri. Kwa kawaida ndege hiyo hubeba abiria 12.
Mashuhuda waliokuwa eneo la tukio wamelielezea tukio hilo kuwa la kusikitisha sana, na kuna madai kuwa baadhi yao waliwapungia mikono wafanyakazi wa ndege hiyo kabla ya janga hilo kutokea.