Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kupiga kura leo kuhusu rasimu mbili za maazimio yanayohusu vita vinavyoendelea nchini Iran na athari zake kwa nchi za Mashariki ya Kati.
Rasimu ya kwanza imewasilishwa na nchi za Ghuba, ikilaani mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya mataifa ya Ghuba pamoja na Jordan na Iran.
Hata hivyo, Russia ambayo ni mshirika wa Iran katika baraza hilo, imewasilisha rasimu mbadala ya azimio. Rasimu hiyo haikutaja moja kwa moja Iran, Israel wala Marekani, bali inalenga kulaani mashambulizi yote dhidi ya raia na kuzitaka pande zinazohusika kusitisha mapigano na kurejea kwenye meza ya mazungumzo.
Hatua hiyo ni ya kwanza kuzingatiwa na Baraza la Usalama tangu lilipofanya mkutano wa dharura muda mfupi baada ya mzozo huo kuzuka.
Akihutubia mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Israel na Marekani dhidi ya Iran, pamoja na mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran dhidi ya nchi za eneo hilo, ni ukiukaji wa Katiba ya Umoja wa Mataifa.