Madalali wa Nyumba Waomba Serikali Kudhibiti Udalali Haramu Unaodaiwa Kufanywa na Raia wa Kigeni

-rickmedia: Lanka Ting

Lanka Ting

2 days ago
rickmedia: madalali-nyumba-waomba-serikali-kudhibiti-udalali-haramu-unaodaiwa-kufanywa-raia-kigeni-878-rickmedia

Madalali wa nyumba katika maeneo ya kifahari ya Masaki na Oysterbay, jijini Dar es Salaam, wameiomba Serikali kuingilia kati na kuchukua hatua kali dhidi ya kile wanachodai kuwa ni biashara haramu ya udalali inayofanywa na raia wa kigeni, hasa kutoka China, bila vibali halali vya kufanya kazi nchini.

Kwa mujibu wa madalali hao, raia hao wa kigeni wamekuwa wakiingia sokoni kwa msaada wa baadhi ya Watanzania, wakiwemo madereva binafsi na wakalimani, kisha kufanya biashara ya udalali kwa kuongeza bei za upangishaji nyumba kwa siri ili kujipatia kamisheni.

"Hali hii inatupokonya wateja wetu wa kila siku na kuvuruga kabisa ushindani wa soko la upangishaji," amesema mmoja wa madalali wakongwe katika eneo la Masaki. "Watu hawa hawana ofisi wala usajili wowote, lakini wanapeta mitaani wakifanya biashara hiyo kama sisi."

Madalali hao wanasema hali hiyo imeathiri kipato chao na kuharibu uaminifu wa soko, huku wakisema baadhi ya wateja wa kimataifa hupendelea kufanya kazi na raia wenzao, bila kuzingatia sheria na taratibu za nchi.

Wanaiomba Serikali kupitia mamlaka husika, zikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Uhamiaji, na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kufanya ukaguzi wa kina na kuwachukulia hatua wale wanaobainika kufanya biashara bila vibali halali.

Wamependekeza pia kuanzishwa kwa mfumo rasmi wa usajili wa madalali pamoja na kudhibiti ushawishi usio rasmi unaofanywa na wageni kwenye soko la nyumba.