Serikali ya Kenya imetangaza rasmi kuwa haiwezi tena kumudu kikamilifu ufadhili wa elimu ya bure katika shule za msingi na sekondari, kutokana na mzigo mkubwa wa kifedha unaosababishwa na ongezeko la idadi ya wanafunzi.
Akizungumza mbele ya Kamati ya Bunge la Kitaifa, Waziri wa Fedha John Mbadi alisema kuwa serikali imelazimika kupunguza fedha zinazotengwa kwa sekta ya elimu. Kwa mujibu wake, ongezeko kubwa la wanafunzi limezidi uwezo wa bajeti ya sasa.
“Kwa sasa, wanafunzi wa shule ya msingi wanapewa ufadhili wa KSh 1,420, shule ya sekondari ya chini ni KSh 15,042, na kwa sekondari ya juu ni KSh 22,244 kwa kila mtoto. Lakini kiwango hiki kitapunguzwa hadi KSh 16,900 kwa mwanafunzi mmoja wa sekondari,” alisema Mbadi.
Aliongeza kuwa kufuatia changamoto za kifedha na vipaumbele vipya serikalini, kuongezwa kwa kiwango cha ufadhili hakitawezekana kwa sasa, lakini linaweza kupitiwa tena endapo mapato ya taifa yataimarika.
Waziri wa Elimu Julius Ogamba aliiunga mkono kauli hiyo akisema, “Katika kipindi cha miaka minne hadi mitano iliyopita, idadi ya wanafunzi imeongezeka kwa kasi ambayo haijawahi kushuhudiwa, lakini bajeti ya wizara ya elimu imebaki palepale.”
Kutokana na hatua hii, mzigo wa kugharamia elimu sasa utabebwa zaidi na wazazi, jambo linalotajwa kuathiri moja kwa moja upatikanaji wa elimu kwa watoto kutoka familia masikini.