Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ametangaza kuwa Ufaransa itatambua rasmi Taifa la Palestina mwezi Septemba katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York.
Ufaransa itakuwa nchi ya kwanza ndani ya kundi la G7 kuchukua hatua hiyo. Kupitia mtandao wa X, Macron amesema hatua hiyo inalenga kusitisha vita Gaza, kuwaokoa raia, na kufanikisha amani ya kudumu.
Ametoa wito wa usitishaji mapigano wa haraka, kuachiliwa kwa mateka wote na msaada mkubwa wa kibinadamu kwa Gaza.
Macron pia ameeleza kuwa uamuzi huo ni sehemu ya msimamo wa muda mrefu wa Ufaransa kuhusu haki ya Wapalestina kuwa na taifa lao, huku akisisitiza ulazima wa kuondolewa kwa Hamas na kulindwa kwa usalama wa Israel.