Jeshi la Polisi mkoani Lindi linamshikilia Araba Samali Chichonyo (57), mkazi wa Kijiji cha Juhudi “A”, Kata ya Chinongwe, Wilaya ya Ruangwa, kwa tuhuma za kumbaka mwanamke mwenye umri wa miaka 78. Tukio hilo la kinyama lilitokea usiku wa Julai 20, 2025, wakati mtuhumiwa na wahanga walipokuwa wakinywa pombe ya kienyeji aina ya wanzuki nyumbani kwa mwanamke huyo.
Chichonyo, aliyekuwa ameajiriwa kuchimba shimo la choo kwa malipo ya TZS 10,000, alitekeleza ukatili huo baada ya kulipwa sehemu ya malipo na kurejea akiwa amelewa. Inadaiwa alitumia nafasi ya mume wa muhanga aliyekuwa mlevi kupoteza fahamu, na ndipo alipoamua kutekeleza kitendo hicho cha udhalilishaji mbele ya mlemavu huyo.
Baada ya tukio, mtuhumiwa alitoroka, lakini alikamatwa baadaye kwa usaidizi wa wananchi. Sasa anashikiliwa na polisi kwa mahojiano na hatua za kisheria.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Lindi amelaani kitendo hicho na kutoa wito kwa jamii kushirikiana na vyombo vya dola katika mapambano dhidi ya ukatili. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuheshimu utu wa binadamu, hasa kwa wazee na watu wasiojiweza.