Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amekanusha madai ya kutofautiana na mkewe Brigitte, baada ya video kuibuka ikionyesha kile kinachoonekana kama mke wa rais wa Ufaransa kumsukuma usoni mumewe walipowasili Hanoi, Vietnam, kwa ziara rasmi.
Macron baadaye aliwaambia waandishi wa habari kuwa yeye na mkewe ambao wameoana tangu mwaka 2007 baada ya kukutana katika shule ya sekondari ambapo yeye alikuwa mwanafunzi na Brigitte alikuwa mwalimu walikuwa wakitania tu.
"Tulikuwa tunataniana, kwa kweli tulikuwa tukicheka na mke wangu," alisema, na kuongeza kuwa tukio hilo limechukuliwa kwa uzito kupita kiasi: "Inageuka kuwa kama janga la sayari nzima."
Aliongeza kuwa video nyingine pia zimefafanuliwa vibaya, kama zile zinazoonyesha madai ya yeye kushiriki mfuko wa kokeini au kumkabili rais wa Uturuki. "Hakuna kati ya haya yaliyo ya kweli," alisema, na "kila mtu anahitaji kutulia."