Mshambuliaji wa Manchester United, Marcus Rashford, amejiunga na Aston Villa kwa mkopo hadi mwisho wa msimu.
Uhamisho huo unakuja baada ya mchezaji huyo kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara chini ya meneja wa sasa wa Manchester United, Ruben Amorim ambaye wameonekana kutokuwa na mahusiano mazuri.
Katika makubaliano ya mkopo huo, Aston Villa itakuwa na chaguo la kumnunua Rashford kwa mkataba wa kudumu kwa dau la pauni milioni 40. Pia, klabu hiyo itachukua jukumu la kulipa asilimia 75 ya mshahara wa Rashford, ambao unakadiriwa kuwa pauni 325,000 kwa wiki.
Rashford (27), amekuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Manchester United tangu alipopandishwa kutoka akademi ya klabu hiyo. Amecheza mechi 426 na kufunga mabao 138 katika mashindano yote akiwa na Manchester United.
Hatua ya Rashford kuondoka United inahusishwa na ukosoaji kutoka kwa meneja Ruben Amorim, ambaye alieleza kutoridhishwa na bidii ya mshambuliaji huyo mazoezini.
Hata hivyo, Rashford ameonyesha furaha yake kujiunga na Aston Villa, akisema kuwa anavutiwa na mtindo wa uchezaji wa klabu hiyo pamoja na malengo yao makubwa.