Kikosi cha Yanga kimeondoka alfajiri ya leo Jumatano Septemba 17, 2025 Dar es Salaam kuelekea Angola kwa ajili ya mchezo wa Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wiliete ya nchini humo.
Safari ya Wananchi imeanzia Dar es Salaam na kupitia Addis Ababa, Ethiopia, ambapo wataunganisha ndege nyingine kuelekea Luanda tayari kwa mchezo huo utakaochezwa Ijumaa kwenye Uwanja wa Novemba 11, Luanda.
Yanga inakwenda kwenye mchezo huo ikiwa na morali kubwa baada ya ushindi wa bao 1-0 walioupata jana jioni dhidi ya Simba katika fainali ya Ngao ya Jamii katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, bao pekee likifungwa na Pacome Zouzoua.
Timu hizo zinatarajiwa kurudiana Septemba 27 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambapo mshindi wa jumla atakutana na mshindi kati ya Elgeco Plus ya Madagascar na Silver Strikers ya Malawi.