Wasanii wa rap, #Future, #MetroBoomin, na #KendrickLamar wanakabiliwa na kesi ya kisheria kuhusiana na malipo ya mrahaba yasiyolipwa kutokana na sampuli iliyotumika kwenye wimbo wao maarufu wa kumshambulia #Drake, “Like That.”
Rodney O, ambaye wimbo wake wa zamani “Everlasting Bass” ulisampuliwa katika toleo la awali, amefungua kesi akidai kuwa hakulipwa mrahaba aliyoahidiwa na kuwa sampuli hiyo haikupata idhini ipasavyo. Pia anaishtaki familia ya marehemu Barry White, ambaye kazi yake ilisampuliwa katika remix ya “Like That” iliyotolewa na Kanye West.
Kulingana na kesi hiyo, Rodney O anasema alitolewa kwenye orodha ya waandishi wa nyimbo wakati wimbo huo ulipowasilishwa kwa Tuzo za Grammy. Pia anadai hakupatiwa toleo la wimbo lenye mstari maarufu wa Kendrick Lamar.
Mwakilishi wa Metro Boomin aliiambia TMZ kwamba watayarishaji walipata haki za kutumia sampuli hiyo na walimlipa Rodney O kiasi cha dola 50,000. Mwakilishi huyo aliongeza kuwa matatizo mengine yanaweza kuwa yanatokana na familia ya Barry White, ambayo huenda inachelewesha malipo zaidi ya mrahaba kupitia uhusiano wake na Epic Records. Familia hiyo bado haijatoa tamko kuhusu jambo hilo.