Jeshi la Polisi la Jimbo la Pennsylvania limemkamata mwanamume mmoja kutoka Harrisburg wakisema alivunja na kuingia katika makazi ya Gavana Josh Shapiro mapema Jumapili na kuwasha moto wakati Shapiro na familia yake walikuwa wamelala.
Cody Balmer, mwenye umri wa miaka 38, alikamatwa kuhusiana na tuhuma za uteketezaji wa makusudi wa moto huo, ambao ulitokea saa chache baada ya Shapiro na familia yake kuandaa chakula cha jioni cha Pasaka.
Waendesha mashtaka walisema wanapanga kumfungulia Balmer mashtaka ya jaribio la mauaji, ugaidi, uteketezaji mkubwa wa moto na shambulio kubwa dhidi ya mtu mwenye hadhi maalum.
Shapiro, mwenye umri wa miaka 51, alichaguliwa kuwa gavana wa Pennsylvania mwaka wa 2022 baada ya kuhudumu kwa miaka sita kama mwanasheria mkuu wa jimbo.
Akiwa Democrat maarufu, alikuwa mmoja wa wagombea waliotajwa kama mgombea mwenza wa Makamu wa Rais wa zamani Kamala Harris wakati wa kampeni yake ya urais mwaka 2024 na pia ametajwa kama mgombea anayetarajiwa kuwania urais mwaka wa 2028.