Wakati maelfu ya waumini wakiendelea kumiminika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro kumuaga Papa Francis, maandalizi ya kumchagua Papa mpya yameanza kwa kasi jijini Roma.
Mkutano wa Tatu wa Jumuiya ya Makardinali
Asubuhi ya Alhamisi, Makardinali 113 waliokusanyika Roma walifanya mkutano wao wa tatu wa maandalizi, ambapo walifanya maamuzi muhimu yafuatayo:
Padre Donato Ogliari, O.S.B., Abate wa Kanisa la St. Paul Nje ya Kuta, atatoa tafakuri ya kwanza siku ya Jumatatu.
Kardinali Raniero Cantalamessa, Mhubiri Mstaafu wa Nyumba ya Kipapa, atatoa tafakuri ya pili mwanzoni mwa Conclave.
Kardinali Víctor Manuel Fernández atasimamia Misa ya siku ya sita ya Novemdiales, badala ya Kardinali Kevin Farrell.
Ingawa tarehe rasmi ya kuanza kwa Conclave bado haijatangazwa, Makardinali wameanza mijadala ya wazi kuhusu hali ya Kanisa na dunia kwa ujumla. Mkutano unaofuata umepangwa kufanyika Ijumaa saa 3:00 asubuhi.
Maelfu Wamiminika Kumwaga Papa Francis
Kwa mujibu wa Matteo Bruni, Mkurugenzi wa Ofisi ya Habari ya Vatican, hadi saa 7:00 mchana (Alhamisi), waumini 61,000 tayari walikuwa wamepita mbele ya mwili wa Papa Francis katika Kanisa Kuu la Mt. Petro. Kanisa litabaki wazi hadi saa 6:00 usiku, isipokuwa kama kutakuwa na foleni ndefu zaidi.
Mazishi ya Papa Francis
Misa ya mazishi ya Papa Francis itafanyika siku ya Jumamosi, Aprili 26,Sala ya Rozari itaandaliwa mbele ya Basilika ya Mtakatifu Maria Mkuu saa 3:00 usiku siku hiyo.
Mazishi ya Papa yatafanyika kwa faragha, bila umma watu wa nje kushiriki moja kwa moja.
Kuanzia Jumapili, Aprili 27 asubuhi, waumini wataanza kuruhusiwa kutembelea kaburi la Papa Francis katika Basilika hiyo ya Marian.