Idadi ya waliopoteza maisha kufuatia kuanguka kwa paa la ukumbi maarufu wa Jet Set nchini Dominican Republic imefikia 218. Taarifa hizi zilitolewa na Mkurugenzi wa Operesheni za Dharura, Juan Manuel Mendez, ambaye pia alithibitisha kuwa watu 189 waliokolewa wakiwa hai.
“Hatutaacha hadi tumewapata wote, hai au wamefariki,” alisema Mendez kwenye mkutano na waandishi wa habari. Hakuna manusura waliopatikana tangu Jumanne alasiri.
Ukumbi huo ulikuwa umejaa wasanii, wanamichezo na maafisa wa serikali. Mashuhuda walisema kuwa vumbi lilianza kuanguka kutoka juu kabla paa halijaporomoka ghafla.
Wakati juhudi za uokoaji zikigeuka kuwa za kutafuta miili, familia na marafiki wa waliokuwa ndani walikusanyika nje ya Taasisi ya Taifa ya Uchunguzi wa Vifo wakisubiri taarifa za wapendwa wao.
Chanzo halisi cha kuanguka bado hakijajulikana, lakini uongozi wa Jet Set wamesema wanashirikiana na mamlaka. Wizara ya Ujenzi na Ofisi ya Meya hazijatoa tamko lolote rasmi.
Tukio hili limetoa tahadhari kubwa kwa tasnia ya burudani duniani. Ni muhimu kwa wasanii na mashabiki nchini kujiuliza: Je, kumbi za matamasha tunayozitumia zipo salama?
Waandaaji wa matamasha na wamiliki wa kumbi lazima wahakikishe miundombinu yao inafuata viwango vya ujenzi na usalama, ili kuepusha maafa kama haya. Wasanii wetu wana haki ya kufanya kazi katika mazingira salama, kuhakikisha usalama wa mashbiki wanaowafuata kwa wingi.