Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Lindi imemhukumu Salumu Moshi Mkumbwa (20), mkulima kutoka Mtanda, kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mwanafunzi wa kidato cha pili mwenye umri wa miaka 16 na kumsababishia maambukizi pamoja na maumivu makali.
Imeelezwa kuwa kati ya Desemba 2024 hadi Mei 13, 2025, mtuhumiwa alimlaghai mwanafunzi huyo na kufanya naye mapenzi hadi alipobainika na mama mzazi wa mwanafunzi ambaye aliripoti Polisi. Baada ya upelelezi, mtuhumiwa alifikishwa mahakamani na ingawa alikana tuhuma, ushahidi wa vielelezo vinne na mashahidi watano ulimtia hatiani, hivyo kuhukumiwa kifungo hicho.