Serikali ya Albania imeandika historia kwa kumteua Diella, mfumo wa akili bandia (AI), kuwa waziri wa kwanza duniani kusimamia zabuni za umma. Hatua hii inalenga kuondoa rushwa na kuongeza uwazi katika maamuzi ya manunuzi ya serikali.
Diella, iliyotengenezwa na Wakala wa Kitaifa wa Jamii ya Habari, tayari imekuwa ikihudumia wananchi kupitia jukwaa la e-Albania kwa kutoa nyaraka na huduma mbalimbali mtandaoni. Waziri Mkuu Edi Rama alisema AI huyo hawezi kuhongwa, haina ajenda ya kisiasa, na itaanza kushughulikia michakato ya zabuni hatua kwa hatua, ikiwa sehemu ya mageuzi ya kupambana na ufisadi kuelekea malengo ya Albania kujiunga na Umoja wa Ulaya.
Hata hivyo, wapo wakosoaji wanaouliza kuhusu uwajibikaji na uhalali wa uteuzi huo. Wanatahadharisha kuwa taarifa zenye upendeleo, makosa ya programu au hata udukuzi vinaweza kuathiri ufanisi wa Diella. Viongozi wa upinzani pia wanapinga kikatiba nafasi ya AI kama waziri.
Ufanisi wa Diella utapimwa kwa kiwango ambacho wananchi na viongozi wataamini teknolojia hii mpya katika kulinda maslahi ya umma.