Mgombea urais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina, amewasili katika Ofisi za Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) leo, Jumamosi, Septemba 13, 2025, kwa ajili ya kurejesha fomu ya uteuzi wa kugombea nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Amewasili katika ofisi hizo akiambatana na mgombea mwenza wake, Fatma Abdulhabib Fereji na viongozi mbalimbali wa ACT-Wazalendo, akiwemo Kiongozi wa Chama, Dorothy Semu.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku mbili tu tangu aliposhinda kesi dhidi ya INEC, kufuatia shauri la maombi ya kikatiba alilowasilisha kupinga hatua ya kuenguliwa kwenye mchakato wa uteuzi wa wagombea wa urais.
Agosti 26, 2025, INEC ilimzuia Mpina kurejesha fomu na kumwengua kwenye kinyang’anyiro hicho, hatua iliyomlazimu, kwa kushirikiana na Bodi ya Wadhamini ya ACT-Wazalendo, kufungua kesi dhidi ya INEC na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mahakama Kuu katika uamuzi wake imewapa haki Mpina na Bodi ya ACT Wazalendo ikisema Katiba ilikuwa imekiukwa.