Mwimbaji maarufu wa nyimbo za Injili kutoka Rwanda, Gloriose Musabyimana, anayefahamika zaidi kwa jina lake la kisanii Gogo Gloriose, amefariki dunia nchini Uganda akiwa na umri wa miaka 36. Taarifa zinasema kuwa msanii huyo aliaga dunia usiku wa Septemba 3, 2025, baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Kwa mujibu wa watu wa karibu, Gogo alikuwa Uganda kwa ziara ya kikazi iliyoanza mnamo Agosti 28, ambapo alishiriki katika tamasha la muziki wa Injili lililofanyika jijini Mbarara kuanzia Agosti 29 hadi 31. Baada ya tamasha hilo, kikundi chake kilisafiri kuelekea Kampala kwa ajili ya mikutano ya kijamii na shughuli nyingine za huduma.
Hata hivyo, mara baada ya kuwasili Kampala, Gogo alianza kuhisi hali ya kuchoka sana na kuonyesha dalili za kuumwa. Alikimbizwa hospitalini, lakini juhudi za madaktari kumuokoa hazikuzaa matunda, na alifariki dunia usiku huohuo.
Gogo alianza muziki wake kupitia kwaya ya kanisa la Anglican katika eneo la Rwamagana, Mashariki mwa Rwanda. Umaarufu wake ulianza kuongezeka kupitia mitandao ya kijamii, hasa baada ya wimbo wake wa Injili “Everyday, I Need Blood of Jesus” kusambaa mtandaoni mapema mwaka 2024.
Wimbo huo uliwavutia watu wengi duniani, na hatimaye mtayarishaji wa muziki kutoka Afrika Kusini, The Kiffness, aliuchukua na kuutayarisha upya, huku akishirikisha sauti na ala za muziki za kisasa. Toleo hilo lilizidi kuupa wimbo huo umaarufu, na Gogo alipata gawio la haki miliki (royalties) kutokana na matumizi hayo.
Mbali na huo, aliwahi pia kutoa wimbo wa Krismasi uitwao “Uwo Mwana”, ambao ulipokewa vyema na wapenzi wa muziki wa Injili ndani na nje ya Rwanda.