Cardi B Ashinda Kesi iliyokuwa Ikimkabili

-rickmedia: Lanka Ting

Lanka Ting

2 days ago
rickmedia: cardi-ashinda-kesi-iliyokuwa-ikimkabili-963-rickmedia

Msanii maarufu wa muziki wa hip hop, Cardi B (jina halisi Belcalis Almanzar), ameibuka mshindi katika kesi ya madai iliyofunguliwa dhidi yake na aliyekuwa mlinzi wake wa usalama, Emani Ellis, ambaye alidai kushambuliwa na kutukanwa na rapa huyo mwaka 2018.

Katika kesi hiyo iliyosikilizwa katika Mahakama ya Jiji la Los Angeles, Ellis alitaka fidia ya Dola za Marekani milioni 24 (takribani Shilingi bilioni 59.9 za Tanzania), akidai kuwa alipatwa na madhara ya kimwili na kisaikolojia kufuatia tukio hilo ambalo lilitokea nje ya kliniki ya afya ya wanawake (OB/GYN) huko Beverly Hills.

Hata hivyo, majaji walimwachia Cardi B huru baada ya ushahidi kuonesha kuwa hakukuwa na shambulio lolote la kimwili. Mashahidi kadhaa, wakiwemo wafanyakazi wa kliniki na daktari aliyekuwa akimhudumia Cardi B wakati huo, walikanusha madai hayo ya Ellis. Uamuzi wa jopo la majaji 12 uliupinga kwa kauli moja upande wa mlalamikaji.

Cardi B, ambaye alihudhuria vikao vyote vya kesi hiyo, alielezea furaha yake baada ya hukumu kutolewa, na kutoa onyo kwa wale wanaopanga kumfungulia kesi zisizo na msingi.

"Sasa mtu yeyote atakayejaribu kuniwekea kesi ya uongo, nitafungua kesi ya madai dhidi yake. Watalipa," alisema Cardi B katika mahojiano na waandishi wa habari nje ya mahakama.

Katika hatua ya kujibu ushindi huo, Cardi B ameeleza dhamira yake ya kufungua kesi ya madai dhidi ya Emani Ellis, akilenga fidia ya hasara ya muda, rasilimali na athari ya jina kutokana na kesi hiyo.

Kwa upande wake, Ellis amesema anakusudia kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo, huku akieleza kuwa alisimama kidete kutetea haki zake. Pia ameeleza nia yake ya kujiunga na masomo ya sheria baada ya kupitia changamoto hiyo ya kisheria.